Lugha Nyingine
Rais Xi na mwenzake Biden watumiana salamu za pongezi kwa kuadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia
BEIJING- Rais wa China Xi Jinping na Rais wa Marekani Joe Biden wametumiana salamu za pongezi siku ya Jumatatu kuadhimisha miaka 45 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia wa nchi hizo mbili, ambapo katika ujumbe wake, Rais Xi amesema kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Marekani ni tukio kubwa katika historia ya uhusiano ya nchi mbili na wa kimataifa.
Amesema, katika miaka 45 iliyopita, uhusiano kati ya China na Marekani umepita changamoto na mafanikio mengi na kusonga mbele kwa ujumla, hali hii siyo tu imeimarisha ustawi wa watu wa pande hizo mbili, bali pia imeendeleza amani, utulivu na ustawi wa Dunia.
Historia tayari imethibitisha na itaendelea kuthibitisha vya kutosha kwamba kuheshimiana, kuishi pamoja kwa amani na kufanya ushirikiano wenye manufaa kwa pande zote ni njia sahihi kwa China na Marekani kuendana kwa pamoja zikiwa nchi mbili kubwa, amesema rais wa China.
Amesema, kanuni hizo zinapaswa kuwa mwelekeo wa juhudi za pamoja zinazofanywa na China na Marekani katika zama mpya.
Rais Xi amesema kuwa yeye na Biden, kwenye mkutano wao mjini San Francisco, waliweka "maono ya San Francisco" yenye mwelekeo wa siku za baadaye, wakiweka dira ya maendeleo ya uhusiano kati ya China na Marekani.
Rais Xi amesisitiza kuwa angependa kufanya ushirikiano na Biden ili kuendelea kuongoza maendeleo ya uhusiano kati ya China na Marekani, ili kunufaisha nchi hizo mbili na watu wao, na kuhimiza lengo kuu la amani na maendeleo ya Dunia.
Katika ujumbe wake Biden amesema tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia Mwaka 1979, uhusiano kati ya Marekani na China umewezesha ustawi na fursa za Marekani, China na Dunia.
Amesema amejitolea kusimamia kiwajibu uhusiano huu muhimu, huku akitarajia kuendelea kuendeleza uhusiano wa Marekani na China kwenye msingi wa maendeleo yaliyofikiwa na viongozi watangulizi wa nchi hizo mbili na kupitia mikutano na majadiliano mbalimbali kati ya wakuu hao wa nchi.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma