Lugha Nyingine
Shughuli ya uenezi mtandaoni wa utamaduni wa Mfereji Mkuu wa China yazinduliwa Jiangsu, China
Katika kuadhimisha miaka 10 tangu Mfereji Mkuu wa China uorodheshwe kwa mafanikio kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia, shughuli ya uenezi mtandaoni yenye kauli mbiu ya “Urithi wa China, Mfereji Mkuu wa Miaka Elfu” iliyodhaminiwa kwa pamoja na Ofisi ya Kamati Kuu ya Mambo ya Mtandao wa Intaneti ya China, Idara ya Mabaki ya Kale ya Kitamaduni ya China, gazeti la People's Daily, na Kamati ya Mambo ya Mtandao wa Intaneti ya Serikali ya Mkoa wa Jiangsu wa China imezinduliwa rasmi huko Yangzhou, Mkoa wa Jiangsu wa China tarehe 22, Juni.
Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati Kuu ya Mambo ya Mtandao wa Intaneti ya China Zhuang Rongwen amesema kuwa, mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 10 tangu ombi la Mfereji Mkuu wa China kuorodheshwa kwenye Orodha ya Urithi wa Dunia lipitishwe kwa mafanikio.
Amesema, ni muhimu kuwezesha uenezi wa utamaduni wa mfereji huo kwa kutumia intaneti, kuhimiza na kuendeleza urithi huo wa utamaduni katika zama mpya, na kuufanya “mshipa” huo wa maji wenye historia ya miaka elfu utiririke kuelekea siku za baadaye na duniani.
Mhariri mkuu wa gazeti la People's Daily Yu Shaoliang amesema, ni muda mwafaka mwaka huu, kwa pamoja kufanya hafla ya uzinduzi wa shughuli hiyo kwenye mji wa Yangzhou, ambao ni mji ulioongoza kazi ya ombi hilo la kuorodheshwa kwenye orodha ya urithi wa Dunia kwa mfereji mkuu. Amesema, shughuli hiyo itawezesha uzuri wa utamaduni wa jadi wa China ufikie watu wengi zaidi, hasa vijana.
Shughuli hiyo pia ilizindua miradi mbalimbali ya vyombo vya habari, na kutangaza matokeo muhimu ya kiakiolojia yaliyogunduliwa kwenye sehemu ya Jiangsu ya mfereji huo mkuu katika miaka hiyo 10 iliyopita.
Watu zaidi ya 300 kutoka Ofisi ya Kamati Kuu ya Mambo ya Mtandao wa Intaneti ya China, Idara ya Mabaki ya Kale ya Kitamaduni ya China, maafisa wa serikali ya Mkoa wa Jiangsu na Mji wa Yangzhou, wahusika wa People’s Daily, na waandishi habari wengi wameshiriki kwenye shughuli hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma