Lugha Nyingine
Eneo maalum la zamani la Viwanda lajizatiti kustawi tena kupitia uvumbuzi
Picha iliyopigwa Agosti 1, 2024 ikionesha vifaa vya kisasa vikiwa kwenye “Shamba linalojisimamia bila ya Binadamu” katika eneo la kielelezo la kitaifa la viwanda vya teknolojia ya hali ya juu ya kilimo la Changchun lililopo Changchun, Mkoa wa Jilin, Kaskazini Mashariki mwa China. (Xinhua/Li He)
Mchana wenye joto kali wa siku moja ya Julai, mjini Changchun, mji mkuu wa Mkoa wa Jilin, moja ya maeneo kiini cha kilimo ya China, mapinduzi ya kimyakimya yalikuwa yakijitokeza, yakibadilisha taswira ya zama za zamani ya wakulima kufanya kazi kwa kutumia nguvu nyingi chini ya jua kali.
Katika tambarare pana, mashamba ya mahindi yameenea mpaka upeo wa macho, huku vishada vikiashiria muda wa kufanya usimamizi wa mashamba. Hata hivyo, hakuna mkulima hata mmoja anayeonekana shambani.
Ghafla droni yenye mabawa ya zaidi ya mita moja ilitokea juu ya mashamba hayo ya mahindi, ikiacha nyuma ukungu wa dawa ya kuua wadudu iliyonyunyizia huku ikiruka kuelekea mbali. Mashamba hayo yalikuwa yamefungwa vifaa vya kisasa vyenye ufanisi, kimyakimya vikikusanya, kuchambua na kuhifadhi data kuhusu unyevunyevu wa ardhi, wadudu, hali ya ukuaji wa mazao na hatari zinazowezekana kutokea.
Hilo ni “Shamba linalojisimamia bila ya binadamu” kwenye eneo la kielelezo la kitaifa la viwanda vya teknolojia ya hali ya juu vya kilimo la Changchun. Katika eneo hilo la mradi, mchakato mzima wa kilimo, kuanzia kulima na kupanda hadi usimamizi na kuvuna, hufanywa na mashine za kilimo za kiotomatiki zinazoongozwa na Mfumo wa Satelaiti wa Beidou.
“Huu ni mustakabali wa kilimo nchini China, na lengo letu ni kuufanya kuwa uhalisia kwa mashamba yote mapema iwezekanavyo,” Yu Rui, msomi wa Akademia ya Sayansi ya China (CAS) inayoendesha mradi huo amesema, akiwa amesimama mbele ya skrini kubwa ya uangalizi.
Katika Shamba hilo, Yu na wenzake wanajaribu njia mpya za kilimo cha mzunguko, ili kuendeleza mifumo endelevu na himilivu ya kilimo. Njia hizo, pamoja na nyingine zilizovumbuliwa na vyuo vikuu na taasisi nchini kote China zinaoneshwa kwenye eneo lililotengwa maalum la mu 500 (takriban hekta 33.3) ndani ya eneo hilo la kielelezo.
“Tunawaalika mara kwa mara wakulima kutembelea ‘ukumbi huu wa maonesho’ kwa ajili ya mbinu mpya na mbegu bora. Halafu wanaweza kuamua ni mbegu na mbinu ipi itatumika katika mashamba yao,” ameeleza Cai Hongguang, naibu mkuu wa kamati ya usimamizi wa eneo hilo la kielelezo.
Picha hizi za kuunganishwa zilizopigwa Agosti 1, 2024 zikionesha vifaa vya kisasa katika “Shamba linalojisimamia bila ya binadamu” kwenye eneo la kielelezo la kitaifa la viwanda vya teknolojia ya hali ya juu vya kilimo la Changchun huko Changchun, Mkoa wa Jilin, Kaskazini Mashariki mwa China. (Xinhua/Li He)
Picha iliyopigwa Agosti 1, 2024 ikionesha “Shamba linalojisimamia bila ya binadamu” kwenye eneo la kielelezo la kitaifa la viwanda vya teknolojia ya hali ya juu vya kilimo la Changchun huko Changchun, Mkoa wa Jilin, Kaskazini Mashariki mwa China. (Xinhua/Li He)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma