Lugha Nyingine
Maombi ya China ya hataza za kijani yafikia zaidi ya 50% na kuongoza duniani
Abiria wakipanda basi linalotumia umeme la kampuni ya magari ya BYD mjini Cape Town, Afrika Kusini, Februari 28, 2024. (Picha na Xabiso Mkhabela/Xinhua)
BEIJING - Mchango uliotolewa na China kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Dunia umeonekana kwenye ongezeko kubwa la hataza zake, huku ripoti ya hivi karibuni ya Mamlaka ya usimamizi wa Hakimiliki ya Ufunifu ya China ikisema kuwa China imepata nafasi ya kwanza katika idadi ya maombi yaliyotolewa ya hataza za teknolojia za kijani na zenye kutoa kaboni chache mwaka 2023, ambapo ongezeko la mwaka huo lilifikia asilimia 20 na ikichukua zaidi ya nusu ya maombi hayo ya jumla duniani.
Ongezeko hili ni asilimia 7.1 ya pointi zaidi ya wastani wa yale ya duniani, mamlaka hiyo imesisitiza katika Ripoti ya Uchambuzi wa takwimu za Hataza za Teknolojia za Kijani na zenye Kutoa Kaboni Chache.
Ripoti hiyo inafafanua hataza za kijani na kaboni chache kuwa ni zile teknolojia ambazo zinaweza kuhimiza maendeleo ya kijani. Hizi hujumuisha maeneo matano muhimu -- upunguzaji wa kaboni ya nishati ya visukuku, uokoaji, uchakataji na utumiaji wa nishati, nishati safi, uhifadhi wa nishati, na unasaji, matumizi na uhifadhi wa gesi chafuzi.
Picha iliyopigwa kwa droni tarehe 16 Julai 2024 ikionyesha kituo cha kuhifadhi nishati ya jua katika Wilaya ya Guazhou, Mkoa wa Gansu, Kaskazini Magharibi mwa China. (Xinhua)
China imefanya vyema katika nyanja ya kuhifadhi nishati, ikifikia maombi 37,000 ya hataza mwaka 2023 peke yake, ikichukua asilimia 48 ya idadi ya maombi hayo duniani.
Kuhusu nishati safi, idadi ya maombi ya China ya hataza za uvumbuzi kwa nishati za jua na hidrojeni ilikuwa ya juu zaidi duniani, ikifikia 8,000 na 5,000, mtawalia.
Idadi ya maombi ya China ya teknolojia za kijani na zenye kutoa kaboni chache kupitia Mkataba wa Ushirikiano wa Hataza, ambao ni mfumo wa kimataifa wa ulinzi wa hataza, ilikuwa imezidi 5,000 mwaka 2023, na kupata nafasi ya kwanza duniani kwa mwaka wa tatu mfululizo, ripoti hiyo imesema.
Hasa, China imekuwa nchi inayoongoza duniani kwa kuandikisha maombi ya hataza tangu Mwaka 2019, kwa mujibu wa Shirika la Haki Miliki ya Ubunifu Duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma