Lugha Nyingine
Mahakama ya Kikatiba ya Thailand yavunja chama kikuu cha upinzani cha Move Forward
Pita Limjaroenrat (Kati), kiongozi wa zamani wa Chama cha Move Forward cha Thailand, akiwasili kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Bangkok, Thailand, Agosti 7, 2024. (Xinhua/Rachen Sageamsak)
BANGKOK - Mahakama ya Kikatiba ya Thailand imekivunja chama kikuu cha upinzani cha Move Forward jana siku ya Jumatano, ikiamua kuwa juhudi za chama hicho za kurekebisha sheria dhidi ya kukashifu familia ya kifalme zilikiuka katiba ya nchi hiyo.
Majaji waliosikiliza kesi hiyo walipiga kura kwa kauli moja kuamuru kuvunjwa kwa Chama cha Move Forward na kupiga marufuku wajumbe 11 wa bodi tendaji ya chama hicho kujihusisha na shughuli za kisiasa kwa miaka 10.
Kampeni ya chama hicho ya kurekebisha sheria ya kutukana familia ya kifalme imechukuliwa kuwa jaribio la kuhujumu utawala wa katiba ya kifalme, mahakama hiyo imesema.
Wabunge sita wa chama hicho ambao hapo awali walikuwa wajumbe wa bodi tendaji ya chama hicho kilichovunjwa sasa wamepoteza hadhi yao ya kuwa wabunge, wakiwemo viongozi wa zamani wa chama Pita Limjaroenrat na Chaithawat Tulathon, pamoja na Naibu Spika wa Bunge la Thailand, Padipat Suntiphada, kwa mujibu wa uamuzi huo wa mahakama.
Pita amesema baada ya uamuzi huo kuwa, kundi hilo litaendelea na ajenda zake za kisiasa licha ya kutokuwepo kwake, kwani taarifa za chama kipya zitatolewa kesho Ijumaa.
"Nitahakikisha kwamba ninapitisha kijiti kwa kizazi kijacho cha viongozi," ameuambia mkutano na waandishi wa habari.
Kuvunjwa kwa chama hicho kumekuja baada ya Tume ya Uchaguzi nchini humo kuiomba Mahakama ya Kikatiba kukifuta chama cha Move Forward kufuatia uamuzi wa mahakama hiyo mwezi Januari ulioamuru chama hicho kusitisha juhudi zozote zinazolenga kufuta au kurekebisha sheria ya kutukana familia ya kifalme.
Sheria dhidi ya kukashifu ufalme, au Kifungu cha 112 cha Sheria ya Makosa ya Jinai ya Thailand, kinasema kwamba yeyote anayekashifu, kutusi au kumtishia mfalme, malkia, warithi watarajiwa wa kiti cha ufalme au umalkia ataadhibiwa kwa kifungo cha miaka mitatu hadi 15.
Chama cha Move Forward kiliibuka kuwa chama kikubwa zaidi katika baraza la chini la Bunge katika uchaguzi mkuu wa Thailand mwaka jana, lakini mgombea wake wa nafasi ya waziri mkuu alikosa kuungwa mkono na wabunge wengi.?
Pita Limjaroenrat (Kati), kiongozi wa zamani wa Chama cha Move Forward cha Thailand, akizungumza na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya chama hicho mjini Bangkok, Thailand, Agosti 7, 2024. (Xinhua/Rachen Sageamsak)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma