Lugha Nyingine
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ahimiza kuimarishwa kwa uwakilishi mkubwa wa Afrika katika Baraza la Usalama
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres (Kati) akizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Mei 23, 2024. (Loey Felipe/Picha ya Umoja wa Mataifa/Xinhua)
UMOJA WA MATAIFA - Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa kuimarishwa kwa uwakilishi mkubwa wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuhakikisha kuwa baraza hilo lina "uaminifu na uhalali kamili."
Katika hotuba yake siku ya Jumatatu katika mjadala wa ngazi ya juu wa "Kushughulikia Udhalimu wa Kihistoria na Kuimarisha Uwakilishi MKubwa wa Afrika katika Baraza la Usalama," Guterres amesema Baraza la Usalama limekuwa nguzo ya amani na usalama duniani tangu Mwaka 1945, lakini nyufa katika msingi wake zinazidi kuwa "kubwa sana hata haziwezi kupuuzwa."
"Zinasababisha kugonga mwamba, kukwama na kusimama karibia migogoro mikubwa ya leo," na zinasaidia kuongezeka kwa "mgogoro mpana wa imani na uhalali ambao unaathiri mfumo wenyewe wa ushirikiano wa pande nyingi," amesema.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa dunia imebadilika, lakini muundo wa baraza hilo "haujaendana na mabadiliko."
"Hatuwezi kukubali kwamba chombo kikuu cha amani na usalama duniani kinakosa sauti ya kudumu kwa bara lenye watu zaidi ya bilioni ... wanaochukua asilimia 28 ya nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa," amesema.
"Wala hatuwezi kukubali kwamba maoni ya Afrika hayathaminiwi katika masuala ya amani na usalama, barani humo na duniani kote," amesema.
Mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa Afrika ina uwakilishi mdogo katika miundo ya usimamizi wa dunia, lakini inawakilishwa kupita kiasi katika changamoto ambazo miundo hii imeundwa kushughulikia. "Migogoro, hali ya dharura na migawanyiko ya siasa za kijiografia ina athari kubwa kwa nchi za Afrika."
Guterres ametoa wito kwa nchi zote wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhudhuria Mkutano wa Kilele wa Siku za Baadaye mwezi Septemba, na kuchangia maoni na mawazo yao ili "sauti za Afrika zisikike, mipango ya Afrika iungwe mkono, na mahitaji ya Afrika yatimizwe."
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma