Lugha Nyingine
Watoto milioni 3.4 wako?katika hatari kubwa ya magonjwa ya kuambukizwa?nchini Sudan: UNICEF
Picha iliyopigwa Julai 26, 2024 ikionyesha watu wakiwa kwenye eneo lililofurika maji katika Mji wa Kassala, Mashariki mwa Sudan. (Picha na Mohamed Osman Al-Zain/Xinhua)
KHARTOUM - Watoto takriban milioni 3.4 wenye umri chini ya miaka mitano wako katika hatari kubwa ya kupatiwa magonjwa ya kuambukizwa nchini Sudan, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limesema siku Jumanne katika taarifa yake.
Kutokana na mvua kubwa na mafuriko nchini humo, magonjwa kama vile kipindupindu, malaria, homa ya dengue, surua na rubela "yanaweza kuenea kwa kasi zaidi na kuifanya hali ya watoto kuwa mbaya zaidi katika majimbo yaliyoathirika na kwingineko," Mwakilishi wa UNICEF nchini Sudan Sheldon Yett amenukuliwa akisema katika taarifa hiyo.
Majanga hayo yanatokana na kushuka kwa kiwango kikubwa kwa utoaji wa chanjo na uharibifu wa miundombinu ya afya, maji, vyoo na usafi kutokana na mgogoro wa ndani unaoendelea, amesema, huku akiongeza kuwa kuzorota kwa hali ya lishe ya watoto wengi nchini Sudan kunawaweka katika hatari kubwa zaidi.
UNICEF iliwasilisha dozi 404,000 za chanjo dhidi ya kipindupindu kwa Sudan Septemba 9, imesema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa UNICEF, utoaji wa chanjo nchini Sudan umeshuka hadi asilimia 50 kutoka asilimia 85 ya awali kabla ya kuanza kwa mgogoro huo wa ndani.
Asilimia zaidi ya 70 ya hospitali katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro hazifanyi kazi, na wafanyakazi wa huduma ya afya walio mstari wa mbele hawajalipwa kwa miezi kadhaa, imesema.
Tangu kuzuka kwa mapigano kati ya Vikosi vya Wanajeshi wa Sudan na Vikosi vya Mwitikio wa Haraka mwezi Aprili 2023, magonjwa ya kuambukizwa kama vile kipindupindu, malaria, surua na homa ya dengue yameenea, na kusababisha watu wengi kwa mamia kufariki. Mgogoro huo umesababisha vifo vya watu angalau 16,650 na mamilioni ya watu kukimbia makazi yao.
Waziri wa Afya wa Sudan Haitham Mohamed Ibrahim alitangaza rasmi mlipuko wa kipindupindu nchini humo Agosti 17. Wizara hiyo imehusisha hali ya kuenea kwa kipindupindu na kuzorota kwa hali ya mazingira kunakosababishwa na vita na matumizi ya maji machafu.
Wizara ya Afya ya Sudan imesema siku ya Jumanne kwamba visa 10,022 vya kipindupindu, ikiwa ni pamoja na vifo 328, vimerekodiwa nchini humo kati ya Julai 15 na Jumatatu ya wiki hii.
Picha iliyopigwa Julai 26, 2024 ikionyesha watu wakiwa kwenye eneo lililofurika maji katika Mji wa Kassala, Mashariki mwa Sudan. (Picha na Mohamed Osman Al-Zain/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma