Lugha Nyingine
Viongozi wa dunia wapongeza kupitishwa kwa makubaliano katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Siku za Baadaye
Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva (kwenye mimbari) akizungumza katika Mkutano wa Kilele wa Siku za Baadaye kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 22, 2024. (Xinhua/Li Rui)
UMOJA WA MATAIFA - Wakati Mkutano wa kilele wa Siku za Baadaye ukiingia siku yake ya pili na ya mwisho kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Mareakni siku ya Jumatatu, viongozi kutoka nchi wanachama wa shirika hilo la dunia wameendelea kupongeza kupitishwa kwa Makubaliano ya Siku za Baadaye, huku Makubaliano ya Kimataifa ya Kidijitali na Azimio kuhusu Vizazi Vya Siku za Baadaye yakiwa randama zake.
Makubaliano hayo na randama zake yanajikita katika mambo mbalimbali yakiwemo amani na usalama, maendeleo endelevu, mabadiliko ya tabianchi, ushirikiano wa kidijitali, haki za binadamu, jinsia, vijana na vizazi vya siku za baadaye na mageuzi katika utawala wa kimataifa.
"Mkutano wa Siku za Baadaye ni shughuli ya ngazi ya juu, inayoleta viongozi wa dunia pamoja ili kujenga mapatano mapya ya kimataifa kuhusu jinsi tunavyowezesha siku bora za sasa na kulinda siku za baadaye," shirika hilo la dunia limesema katika taarifa yake kwa umma.
"Fursa hii ya mara moja katika kizazi inatumika kama wakati mzuri wa kurekebisha imani iliyopungua na kuonyesha kwamba ushirikiano wa kimataifa unaweza kukabiliana na changamoto za sasa na vile vile ambazo zimeibuka katika miaka ya hivi karibuni au ambazo ziko karibu kutokea." inasomeka taarifa hiyo.
Rais wa Angola Jo?o Louren?o amesema kuwa kupitishwa kwa Makubaliano ya Siku za Baadaye kunawakilisha "hatua halisi ya mabadiliko" kwa mtazamo wa hamasa, jumuishi na wenye uthubutu zaidi kwa masuala ambayo yanahusu binadamu."
Rais wa Jamhuri ya Czech Petr Pavel amesema kuwa Makubaliano ya Siku za Baadaye yanaunda msingi thabiti wa mfumo bora na wenye ufanisi zaidi wa kimataifa. Hasa, amesisitiza, ni muhimu "kuchangia uelewa wetu wa pamoja wa jinsi ya kushughulikia teknolojia kwa usalama kila siku na kujilinda dhidi ya matumizi yake mabaya ya wenye nia mbaya."
Rais wa Ecuador Daniel Noboa amesema kuwa maamuzi na dhamira zote za kimataifa lazima ziamuliwe kwa "kuhusika na mchango wa wale ambao leo wanaweza kuijenga kesho."
Viongozi wengine waliozungumza sana kuhusu makubaliano hayo, ni pamoja na; Rais wa Tajikistan Emomali Rahmon, Albert II, Mwanamfalme wa Monaco, Waziri Mkuu wa Nepal KP Sharma Oli ambaye alizungumza kwa niaba ya nchi zenye maendeleo ya chini, Rais wa Namibia Nangolo Mbumba, Olaf Scholz, kansela wa Ujerumani, Rais wa Brazil Luiz Inacio Lula da Silva na wengine wengi.
Rais wa Namibia Nangolo Mbumba (kwenye mimbari) akizungumza katika Mkutano wa Kilele wa Siku za Baadaye kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Septemba 22, 2024. (Xinhua/Li Rui)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma