Lugha Nyingine
Kulima ardhi, kugusa mioyo ya watu: Moyo wa Kujitoa kwa profesa wa kilimo wa China kwa Afrika
Profesa Hai Jiangbo akizungumza na Ngnadong Wansim Aboubakar, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu kutoka Cameroon, katika Chuo cha elimu ya kilimo, Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Kaskazini-Magharibi mjini Yangling, Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini Magharibi mwa China, Septemba 3, 2024. (Xinhua/Shao Rui)
XI'AN - Kufuatia safari yake ya 27 katika Bara la Afrika mwezi Januari mwaka huu, Hai Jiangbo, profesa wa kilimo mwenye umri wa miaka 58, anawazia maisha yake baada ya kustaafu miaka michache kutoka sasa: ana matumaini ya kurejea Afrika kuanzisha kituo cha kilimo.
Kwenye safari yake hiyo ya Januari, Hai, mwalimu wa Chuo cha elimu ya kilimo, Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Kaskazini Magharibi, alitumia siku 20 kuwa nchini Guinea. Huko, alisaidia kuandaa mipango ya kina ya maendeleo ya kilimo, akihamasisha nchi hiyo kuanzisha utambulisho maalum wa kilimo kupitia chapa thabiti na upangaji wa kimkakati wa uzalishaji wa kilimo.
Uhusiano wa Profesa Hai na Afrika ulianza rasmi mwaka 2003 alipojiunga na kundi la tatu la waelimishaji wa China waliotumwa Ethiopia kama sehemu ya mpango wa kufundisha.
Awali akiwa amepewa jukumu la kufundisha elimu ya maumbile ya mimea na ikilojia ya kilimo, alifundisha katika darasa mchanganyiko la wanafunzi wenye umri kati ya miaka 12 hadi 45. Licha ya kutopatikana sana kwa intaneti na umahiri wake mdogo wa Kiingereza, alitafsiri kwa bidii vitabu vya Kichina kwenda Kiingereza. Juhudi hizi za mwaka mzima ni mwanzo wa uhusiano wake mkubwa na Afrika.
Katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, ari ya Profesa Hai kwa kilimo cha Afrika imeendelea kuwa yenye hamasa kubwa. Amehusika katika miradi mingi ya misaada kutoka Ethiopia hadi Tanzania, Kenya hadi Madagascar. Kwa kila mradi, ameleta aina mbalibmali za kilimo, teknolojia, dhana na usimamizi uliofanikiwa wa kilimo wa China kwenda Afrika.
Kwa mfano, nchini Cameroon, Hai alikuwa mtu muhimu katika kuongeza mavuno makubwa ya mpunga wa kienyeji hadi kufikia tani 7 kwa kila hekta kwenye mashamba ya kielelezo yenye ukubwa wa hekta takriban 2 kwa kujumuisha baadhi ya mbinu za kilimo cha mpunga.
Zaidi ya kuimarisha maendeleo ya kilimo, Profesa Hai pia amechochea shauku ya elimu ya kilimo miongoni mwa wanafunzi wa Afrika. Katika kipindi cha miaka 21, ametembelea nchi 13 za Afrika, akishauri na kufunza wanafunzi zaidi ya 10,000 wa Afrika katika shahada za uzamili na uzamivu, mafundi wa kilimo, na maafisa wa serikali kupitia vipindi mbalimbali vya mtandaoni na ana kwa ana.
Kwa Profesa Hai, Afrika ni pepo ya maendeleo ya kilimo, iliyobarikiwa kuwa na maliasili nyingi, hali mwafaka ya mwanga na joto, mvua ya kutosha, mitandao mikubwa ya mito pamoja na ardhi kubwa.
Baada ya kustaafu, Hai anapanga kurejea Afrika na kuanzisha vituo vya majaribio, mashamba au jumuiya za ushirika pamoja na wanafunzi wake Waafrika. Anatamani kutekeleza uzoefu zaidi wa kilimo wa China barani Afrika.
"Pamoja na wanafunzi wangu, ninatamani kutoa mchango kwa maendeleo ya kilimo ya nchi za Afrika, usalama wao wa chakula na kuboresha hali ya utapiamlo. Nina imani kwamba mustakabali wa jumuiya yenye mustakabali wa pamoja kati ya China na Afrika ni mzuri sana." amesema.
Picha hii iliyopigwa Septemba 3, 2018 ikionyesha Profesa Hai Jiangbo akizungumza na mwanafunzi wa Rwanda Efienne Niyigabas, katika Chuo cha elimu ya kilimo, Chuo Kikuu cha Kilimo na Misitu cha Kaskazini-Magharibi mjini Yangling, Mkoa wa Shaanxi, Kaskazini Magharibi mwa China. (Xinhua/Li Yibo)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma