Lugha Nyingine
Panda wawili kutoka China wawasili Washington, D.C. Marekani
Ndege ya kusafirisha panda wawili ikiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington, D.C., Marekani, Oktoba 15, 2024. (Xinhua/Hu Yousong)
WASHINGTON – Panda wawili, Bao Li na Qing Bao, wamewasili Washington, D.C. siku ya Jumanne, baada saa ya takriban 19 za safari ya ndege kupita Bahari ya Pasifiki kutoka Mkoa wa Sichuan, Kusini Magharibi mwa China.
Ndege maalum ya "FedEx Panda Express" Boeing 777F ilitua kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington, D.C. majira ya saa 4:00 Asubuhi kwa saa za huko (1400 GMT).
Panda hao walipakiwa kwenye malori na kupelekwa kwenye Bustani ya Taifa na Taasisi ya Uhifadhi wa Viumbe ya Smithsonian (NZCBI). Panda hao wenye umri wa miaka mitatu watakuwa na makazi yao mapya katika bustani hiyo ya wanyama, ikiwa ni sehemu ya mpango wa ushirikiano wa kimataifa wa ulinzi wa panda wa miaka 10.
"Timu yetu imefanya kazi bila kuchoka kujiandaa kwa ajili ya kuwasili kwa panda hawa, na tunayo furaha kuwakaribisha Bao Li na Qing Bao Washington, D.C.," Brandie Smith, mkurugenzi wa NZCBI ya John na Adrienne Mars, amesema katika taarifa.
"Ninawashukuru wenzetu wa China kwa jitihada zetu za ushirikiano za uhifadhi na utafiti, kwa upande wa FedEx kwa kuwapa usafiri salama na kwa wafadhili na wanajumuiya wetu ambao michango yao ya hisani inawezesha mpango wetu mkubwa wa uhifadhi wa panda," amesema Smith.
Bao Li, panda dume, ambaye jina lake linamaanisha "hazina" na "nishati" kwa lugha ya Kichina, alizaliwa Agosti 2021. Ana uhusiano maalum na bustani hiyo, kwakuwa ni mtoto wa panda Bao Bao na mjukuu wa panda Tian Tian na Mei Xiang – wote walikuwa wakazi wa zamani wa bustani hiyo.
Qing Bao, panda jike, ambaye jina lake linamaanisha "kijani" na "hazina" kwa lugha ya Kichina, alizaliwa Septemba 2021.
Kwa utaratibu wa kawaida, panda hao watawekwa karantini kwenye nyumba ya panda kwa angalau siku 30, bustani hiyo imesema.
Hii ni mara ya pili mwaka huu kwa China kupeleka panda nchini Marekani. Panda wawili, Yun Chuan na Xin Bao, walipelekwa California kutoka China Juni 27, na kuonyeshwa kwa mara ya kwanza hadharani Agosti 9.
Kreti maalum linalobeba panda mmoja likishushwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington, D.C., Marekani, Oktoba 15, 2024. (Picha na Yang Shuang/Xinhua)
Ndege ya kusafirisha panda wawili ikiwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington, D.C., Marekani, Oktoba 15, 2024. (Xinhua/Hu Yousong)
Mfanyakazi akihamisha kreti maalum linalobeba panda mmoja kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Dulles karibu na Washington, D.C., Marekani, Oktoba 15, 2024. (Picha na Yang Shuang/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma