Lugha Nyingine
Rais Xi aahidi kufungua mlango zaidi China inapotekeleza ahadi za WTO
Rais Xi Jinping wa China akitoa hotuba kwa njia ya video kwenye ufunguzi wa Maonesho ya nne ya Kimataifa ya Uagizaji Bidhaa ya China (CIIE) yanayofanyika Shanghai, Novemba 4, 2021. (Xinhua/Li Xueren)
BEIJING, China - Huku kukidhoofika kwa makubaliano ya kimataifa kuhusu kufungua mlango, Alhamisi ya wiki hii Rais Xi Jinping wa China ametoa ahadi mpya ya kufungua soko la China kwa upana zaidi huku nchi hiyo ikiendelea kutekeleza kikamilifu ahadi zake za kujiunga na Shirika la Biashara Duniani (WTO).
Akibainisha kuwa utandawazi unakabiliwa na upepo mkali, Rais Xi wakati akihutubia ufunguzi wa Maonesho ya nne ya Kimataifa ya Uagizaji wa Bidhaa ya China (CIIE) ameonesha wasiwasi wake juu ya kupungua kwa kiwango cha kufungua milango duniani katika muongo mmoja uliopita.
"Lazima tubaki juu ya mwelekeo uliopo wa utandawazi wa kiuchumi, na kuunga mkono nchi duniani kote kufungua kwa upana zaidi huku tukipinga utetezi wa upande mmoja na kujilinda kibiashara. Hili ni muhimu sana ikiwa tunataka kuupeleka ubinadamu katika mustakabali bora" Xi amesema.
"Kufungua ni alama mahususi ya China ya kisasa" Xi amewaambia maafisa, viongozi wa biashara na wajasiriamali wanaoshiriki katika maonesho ya CIIE ya mwaka huu huko Shanghai.
Kama sehemu ya juhudi za nchi hiyo za kulinda ushirikiano wa kweli wa pande nyingi, Xi amesema China itashikilia msimamo wa mfumo wa biashara wa pande nyingi kama njia kuu ya kuweka sheria za kimataifa, na kulinda utulivu wa minyororo ya viwanda na ugavi duniani.
Amesema China pia itachukua mtazamo shirikishi na wa wazi katika mazungumzo kuhusu masuala ya uchumi wa kidijitali, biashara na mazingira, ruzuku za viwanda na makampuni yanayomilikiwa na serikali.
Ikiwa na idadi ya watu bilioni 1.4 na zaidi ya watu milioni 400 wenye kipato cha kati, China itashiriki fursa za soko na Dunia nzima kupitia hatua kama vile kufungua maeneo zaidi ya vielelezo kwa ajili ya kukuza ubunifu wa biashara ya kuagiza na kukuza biashara ya mtandao ya Njia ya Hariri, Xi amesema.
Kwa mujibu wa Rais Xi, ili kuhimiza ufunguaji mlango wa hali ya juu, China itafupisha zaidi orodha hasi ya uwekezaji kutoka nje, na kufungua mlango kwa utaratibu katika sekta za mawasiliano ya simu, huduma za afya na huduma zingine.
"China italinda kithabiti maslahi ya pamoja ya dunia" amesema, huku akiahidi kuungana kikamilifu katika juhudi za kimataifa za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kulinda usalama wa chakula na nishati, na kutoa msaada zaidi kwa nchi zingine zinazoendelea ndani ya mfumo wa ushirikiano wa Kusini na Kusini.
Mwaka wa 2021 ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu China ijiunge na Shirika la Biashara la Dunia (WTO). Katika miongo miwili iliyopita, juhudi zinazoendelea za nchi katika kufungua mlango zimeleta maendeleo ya China katika hatua mpya na kuingiza msukumo mpya katika uchumi wa Dunia, Xi amebainisha.
"China imetekeleza kikamilifu ahadi zake za kujiunga," Xi amesema.
Kama maonesho ya kwanza duniani yenye lengo la uagizaji bidhaa wa kitaifa, maonesho ya CIIE ya China ambayo yanaanza leo Novemba 5 - Novemba 10, yametoa jukwaa kwa wajasiriamali na wafanyabiashara kote duniani. Maonesho ya CIIE ya mwaka huu yanavutia karibu biashara 3,000 kutoka nchi na maeneo 127, ikiwa ni idadi kubwa kuliko maonesho ya tatu yaliyofanyika mwaka jana wa 2020.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma