Lugha Nyingine
UN yaanza juhudi za kutoa msaada kufuatia mlipuko wa volkano Visiwa vya Tonga
Wataalam wa jiolojia kutoka Tonga wakiwa kwenye meli huku wakitazama mlipuko wa volkano ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai huko Tonga, Januari 15, 2022. (Picha kutoka Taasisi ya Huduma za Jiolojia ya Serikali ya Tonga)
UMOJA WA MATAIFA – Msemaji wa Umoja wa Mataifa (UN), Stephane Dujarric amesema kwamba Chombo hicho cha Dunia na mashirika yake yanatayarisha juhudi za kutoa msaada kwa Tonga, nchi ya visiwa katika Bahari ya Pasifiki Kusini, kufuatia mlipuko wa volkano ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apa.
"Wenzetu wa huduma za kibinadamu na serikali wanaripoti uharibifu mkubwa wa miundombinu karibu na Tongatapu (kisiwa kikuu kwenye Visiwa vya Tonga) na hakuna mawasiliano kutoka visiwa vya Ha'apai," Stephane Dujarric, msemaji mkuu wa Ofisi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema. "Tuna wasiwasi hasa kuhusu visiwa viwili vidogo, Mango na Fonoi, kufuatia ndege za uchunguzi kuthibitisha uharibifu mkubwa wa mali."
Australia na New Zealand zilifanya safari za ndege mwishoni mwa juma lililopita.
Dujarric amesema, ingawa hakukuwa na ripoti za mara moja za vifo au majeruhi kufuatia mlipuko mkubwa wa Jumamosi, watu wawili wameripotiwa kupotea.
Amesema Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linapanga juhudi za kupeleka vifaa vya msaada na wafanyakazi. Shirika hilo linatuma timu yake ya mawasiliano ya dharura ili kusaidia kurejesha njia za mawasiliano nchini Tonga.
Msemaji huyo amesema Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasubiri uthibitisho wa Serikali ya Tonga kabla ya kusafirisha vifaa vya dharura vilivyohifadhiwa kwenye maghala ya Fiji na Brisbane, Australia. Vifaa hivyo ni pamoja na vifaa muhimu vya maji, usafi wa mazingira na mwili, mapipa ya maji na ndoo na vifaa vya kupima maji ardhini, turubai, vifaa vya kuchezea watoto na mahema.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) ilisema tsunami iliyotokea baada ya mlipuko huo mkubwa imeleta uharibifu mkubwa katika fukwe za Magharibi za Tongatapu, na mahoteli na nyumba kadhaa zimebomoka au kuharibika vibaya.
Ofisi hiyo imeeleza kuwa, mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa yanayoshughulikia misaada kwa Tonga ni pamoja na Mfuko wa Idadi ya Watu wa Umoja wa Mataifa, Shirika la Chakula na Kilimo, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji na Shirika la Afya Duniani. Imebainisha kwamba, mashirika hayo yanafanya kazi kwa karibu na mamlaka husika nchini Tonga, washirika wa huduma za kibinadamu na nchi wafadhili.
OCHA imesema, Serikali ya New Zealand na Australia zilitangaza ufadhili wa dharura kwa ajili mwitikio wa haraka wa misaada, na Australia inatayarisha meli kuelekea Tonga ikiwa imebeba vifaa vya misaada.
Ofisi hiyo ya misaada ya kibinadamu ya UN imesema hakuna madhara makubwa kwa visiwa vingine vya Bahari ya Pasifiki vya Fiji, Samoa, Vanuatu na Visiwa vya Solomon ambavyo viko jirani na Tonga licha ya mafuriko.
Picha ya Januari 14, 2022 ikionesha mlipuko wa volkano ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai nchini Tonga. (Picha kutoka Shirika la Huduma za Jiolojia la Serikali ya Tonga)
Picha ya Januari 14, 2022 ikionesha mlipuko wa volkano ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai nchini Tonga. (Picha kutoka Shirika la Huduma za Jiolojia la Serikali ya Tonga)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma