Lugha Nyingine
Rais Xi aagiza kujenga eneo la kurusha vyombo vya kwenda anga ya juu lenye ubora duniani
WENCHANG, Hainan - Rais Xi Jinping wa China ametaka kufanyika kwa juhudi zaidi za kuinua viwango vya eneo la kurushia vyombo vya kwenda anga ya juu katika Mkoa wa Kisiwa cha Hainan Kusini mwa China hadi kufikia viwango vinavyoongoza duniani wakati alipokagua eneo hilo siku ya Jumanne wiki hii.
Xi, ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China na Mwenyekiti wa Kamati ya Kuu ya Kijeshi, ya China ameyasema hayo kwenye eneo la kurushia vyombo vya kwenda anga ya juu la Wenchang.
Katika ziara hiyo, Xi pia ametoa salamu kwa wafanyakazi wote waliopo kwenye eneo hilo na kuwataka kubeba wajibu wao na kuwa wajasiri wa kuvumbua na kukamilisha majukumu kwa mafanikio mapya.
Baada ya kujulishwa kuhusu eneo hilo, Xi alikagua mnara wa urushaji wa vyombo vya kwenda anga ya juu na vifaa vingine. Amezungumza sana juu ya mfululizo wa safari muhimu za anga ya juu zilizoanzia kwenye eneo hilo, ikiwa ni pamoja na kurushwa kwa moduli ya msingi ya Tianhe kwenye kituo cha China cha anga ya juu, safari ya mwezini kwa kutumia chombo cha Chang'e-5, na safari ya utafiti wa Sayari ya Mars kwa kutumia chombo cha Tianwen-1.
Xi ameeleza kuwa Wenchang ni kituo cha kurushia roketi za kizazi kipya za China na kichwa cha nchi katika utafiti wa anga ya juu.
“Eneo la urushaji vyombo linapaswa kuendelea kutilia maanani mipaka ya maendeleo ya anga ya juu ya Dunia na mahitaji makuu ya kimkakati ya sekta ya safari ya anga ya juu ya China, na kuboresha kikamilifu uwezo wake wa kisasa wa kurusha vyombo kwenda anga ya juu”, amesema Xi.
China imepanga kukamilisha ujenzi wa kituo chake cha anga ya juu mwaka huu. Vyombo vya mizigo vya Tianzhou-4 na Tianzhou-5, pamoja na moduli za maabara za Wentian na Mengtian zitarushwa kutoka Wenchang.
Xi amesema eneo la urushaji wa vyombo kwenda anga ya juu linapaswa kufanya juhudi za kina ili kuhakikisha mafanikio kamili ya safari za anga ya juu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma