Lugha Nyingine
Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Duniani lafunguliwa mjini Beijing, China
Washiriki wakipiga picha pamoja kabla ya hafla ya ufunguzi wa Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Duniani Mwaka 2024 mjini Beijing, China, Agosti 12, 2024.(Xinhua/Cai Yang) |
BEIJING – Jukwaa la Maendeleo ya Vijana Duniani Mwaka 2024 limefunguliwa mjini Beijing, China jana siku Jumatatu, huku vijana zaidi ya 2,000 kutoka nchi zaidi ya 130 na mashirika 20 ya kimataifa wakiwa wanashiriki moja kwa moja mtandaoni na ukumbini.
Jumatatu ilikuwa ni Siku ya Kimataifa ya Vijana. Viongozi vijana na wajumbe wa vijana zaidi ya 500 wamekusanyika mjini Beijing kushiriki kwenye ufunguzi wa jukwaa hilo na mkutano wa washiriki wote.
Katika siku zinazofuata, Washiriki pia watatembelea miji mingine ya China, kama vile Nanning na Hangzhou na kushiriki katika majadiliano kuhusu maendeleo ya kijani, maendeleo ya kidijitali, urithishaji wa utamaduni na uvumbuzi, pamoja na kutembelea miji inayolenga maendeleo ya vijana.
Kwenye hafla ya ufunguzi, mtaalamu mkuu wa magonjwa wa China Zhong Nanshan, ambaye pia ni mwanataaluma wa Taasisi kuu ya Uhandisi ya China, alielezea ukuaji binafsi na uzoefu wake wa kazi kwa njia ya video.
Zhong amesema kuwa vijana wamekuwa mstari wa mbele na nguvu kuu katika kukabiliana na matukio ya dharura ya afya ya umma, iwe SARS Mwaka 2003 au janga la hivi karibuni la UVIKO-19.
Zhong amehimiza vijana hao kuwa na matumaini, ndoto kubwa na kujitahidi kupata mafanikio makubwa zaidi katika kuhimiza maendeleo ya teknolojia za mstari wa mbele.
Akitoa hotuba kwa njia ya video, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amesema vijana ndiyo chachu ya Ajenda ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030, na ametoa wito wa juhudi za kufanya sauti zao zisikike na kuwapa haki ya kuonesha uwezo wao kwa kupitia elimu na ujuzi.
Likiwa na kaulimbiu ya " Kujenga Pamoja Siku za Baadaye," shughuli hiyo inatarajiwa kutumika kama tukio muhimu la kuunganisha nguvu za vijana kwa ajili ya kutekeleza Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Maendeleo Endelevu ya Mwaka 2030 na Pendekezo la Maendeleo ya Dunia, mratibu wa jukwaa hilo amesema.
Jukwaa hilo limeandaliwa kwa pamoja na Shirikisho Kuu la Vijana wa China, ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini China na kamati ya maandalizi ya jukwaa hilo. Jukwaa la kwanza la namna hiyo lilifanyika mwaka 2022.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma