Lugha Nyingine
Waziri?wa Mambo ya Nje wa China: China inapinga kuingia kati mambo ya ndani ya?Myanmar
NAY PYI TAW - Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi amesema siku ya Jumatano kwamba China inapinga vikali kuingilia kati mambo ya ndani ya Myanmar na itaendelea kuunga mkono juhudi za Myanmar kuelekea maridhiano ya kisiasa ya ndani chini ya mfumokazi wa kikatiba.
Wang, ambaye pia ni Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), ameyasema hayo alipokutana na Than Shwe, mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Amani na Maendeleo la Serikali ya Myanmar.
Kwenye mkutano huo, Wang amesema China inapinga vikali nguvu za nje kuingilia kati mambo ya ndani ya Myanmar, pamoja na maneno na vitendo vyovyote vinavyodhoofisha utulivu na maendeleo ya nchi hiyo ya Asia Kusini Mashariki.
Wang amesema China itaendelea kuiunga mkono Myanmar katika kulinda uhuru, mamlaka, umoja wa kitaifa na ukamilifu wa ardhi yake na kusisitiza kuwa itaunga mkono juhudi za Myanmar za kufikia maridhiano ya kisiasa ya ndani chini ya mfumokazi wa kikatiba, kufanya uchaguzi na kuanzisha upya mchakato wa mpito wa kidemokrasia.
Kwenye mkutano huo, Than Shwe ameishukuru China kwa kutoa uungaji mkono na msaada wa muda mrefu kwa Myanmar katika nyanja zote.
China ni "paukphaw" (rafiki wa kindugu) na jirani mwema wa Myanmar, na nchi hizo mbili daima zimekuwa zikitendeana kwa njia ya kirafiki, Than Shwe amesema, akibainisha hali ya kuishi pamoja kwa amani kwa muda mrefu kati yao kamwe haitabadilika.
Ameelezea matumaini yake kuwa China itaendelea kutoa uungaji mkono kwa Myanmar, ikiisaidia Myanmar kujilinda dhidi ya uingiliaji kutoka nchi za nje na kudumisha utulivu wa ndani.
Wang alikuwa ziarani nchini Myanmar siku ya Jumatano kabla ya kusafiri kwenda Thailand kuongoza Mkutano wa tisa wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Ushirikiano wa Eneo la Lancang-Mekong na kuhudhuria Mazungumzo Yasiyo Rasmi kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa China, Laos, Myanmar na Thailand.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma