Lugha Nyingine
Nchi za Afrika kushiriki Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China yanayoanza leo (6)
BEIJING - Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara katika Huduma ya China Mwaka 2024 (CIFTIS) yamepangwa kufanyika mjini Beijing kuanzia leo Alhamisi, Septemba 12 hadi Septemba 16, ambapo nchi mbalimbali duniani zikiwemo za Afrika kama vile Nigeria, Ethiopia, Gabon na Burundi zimeweka mabanda yao na kujipanga kushiriki.
Maonyesho hayo yanafanyika siku chache baada ya kumalizika kwa Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika, ambapo makubaliano na hatua mbalimbali za ushirikiano zilitangazwa.
Akizungumza kwenye Banda la Nigeria la Maonyesho hayo Jumatano, siku moja kabla ya kuanza kwa maonyesho hayo, Kaimu Balozi wa Ubalozi wa Nigeria nchini China, Babagana Wakili amesema nchi yake inatarajia kunufaika sana na Maonyesho hayo na imejipanga kutumia Maonyesho hayo kushawishi na kuvutia wawekezaji na wafanyabiashara na vilevile watalii kutoka China
Huku China ikiwa ni nchi yenye soko kubwa linaloibukia, kaimu Balozi huyo amesema, nchi yake itaonesha bidhaa mbalimbali kwenye maonyesho hayo, zikiwemo za mazao kama vile korosho na mihogo, madini, bidhaa za kitamaduni na nyinginezo kwa wateja wa soko hilo la China.
Amesema, China imeendelea kuwa mshirika na rafiki mzuri wa Nigeria na Afrika kwa ujumla ikitoa fursa za uwekezaji, biashara, ujenzi wa miundombinu, ujuzi na teknolojia za kuwezesha kufikia maendeleo.
Ameeleza sera ya Nigeria kwa sasa si kuuza nje bidhaa ghafi bali kuhakikisha bidhaa na mazao mbalimbali ya kilimo yanayouzwa kwenye soko la China na mengineyo yanayotengenezwa kwanza nchini Nigeria na kuuzwa yakiwa bidhaa kamili au katika hali ya kutengenezwa kwa nusu.
Waandaaji wa maonyesho hayo wamesema, nchi ya Ufaransa ndiyo nchi mgeni rasmi wa maonyesho huku Mkoa wa Sichuan wa China ukiwa mkoa mgeni rasmi.
Yakiwa na kaulimbiu ya “Huduma za Kimataifa, Kunufaika Pamoja", maonyesho hayo yatafanyika katika sehemu mbili za Kituo cha Mikutano ya Kitaifa cha China na Bustani ya Shougang mjini Beijing, China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma