Lugha Nyingine
Mabanda ya nchi za Afrika kwenye Maonyesho ya Biashara ya Huduma ya China yavutia kwa kupambwa vizuri, kuwa na bidhaa za kitamaduni
Muonyeshaji bidhaa akipiga ngoma kwenye banda la maonyesho la Rwanda, Septemba 12, 2024 (People’s Daily Online) |
BEIJING - Mabanda ya nchi mbalimbali za Afrika kwenye Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara ya Huduma ya China yameonekana kuvutia kimandhari kwa mapambo ya kupendeza na kuwa na bidhaa za kitamaduni hivyo kufanya watu wengi kuyatembelea kwa hamasa.
Mabanda hayo ambayo yako kwenye ukumbi wa huduma za utamaduni na utalii katika Bustani ya Shougang mjini Beijing chini ya shughuli ndogo ya Maonyesho ya 9 ya Utamaduni ya nchi zinazojenga pamoja "Ukanda Mmoja, Njia Moja" yamepambwa kwa mandhari mbalimbali za kitamaduni, mazingira ya asili na maliasili hivyo kuwa na upekee.
Nchi mbalimbali kama vile Zimbabwe, Uganda, Rwanda, Mali, Tunisia, Morocco, Sudan na Ghana zimeshiriki kwenye shughuli hiyo ndogo ya maonyesho hayo na kuvutia wateja wengi wa China ambao walikuwa na shauku ya kutazama bidhaa hizo, kuulizia bei na hata kuweka miadi na kununua.
Pascal Kofi Ezen muoneshaji bidhaa kutoka Ghana amesema, amekuwa akipokea watembeleaji na wateja kila wakati tangu afungue banda lake na wengi wao wamekuwa wakiulizia bidhaa, kuweka miadi na kubadilishana naye mawasiliano kwa ajili ya majadiliano ya biashara.
Akiwa na matumaini makubwa ya kupata fursa nyingi za biashara yake kwenye maonyesho hayo, Ezen amesema maonyesho hayo ni fursa kubwa kwake kuonesha bidhaa maalum za Ghana kwa wateja wa China na ni fursa ya kujenga ukaribu mkubwa wa nchi yake na China.
Kwa mujibu wa waratibu, maonyesho hayo ambayo yameanza rasmi jana Alhamisi, Septemba 12 na yamepangwa kuendelea hadi Septemba 16 yakiwa na kaulimbiu isemayo “huduma za kimataifa, kunufaika pamoja” yanashirikisha nchi na mashirika ya kimataifa zaidi ya 85 yanayofanya maonyesho na mikutano na kampuni zaidi ya 450 kutoka orodha ya kampuni 500 bora duniani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma