Lugha Nyingine
Biashara ya kimataifa kuongezeka asilimia 2.7 Mwaka 2024: Ripoti ya WTO
Nembo ya Shirika la Biashara Duniani (WTO) ikionekana Geneva, Uswisi, tarehe 5 Aprili 2023. (Xinhua/Lian Yi) |
GENEVA - Kiwango cha biashara ya bidhaa duniani kinatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 2.7 Mwaka 2024, Shirika la Biashara Duniani (WTO) limesema katika ripoti mpya ya Mtazamo wa Biashara na Takwimu za Kimataifa iliyotolewa jana siku ya Alhamisi.
Makadirio hayo ni ya juu kidogo kuliko yale ya awali ya WTO ya ongezeko la asilimia 2.6 yaliyotolewa mwezi Aprili.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, biashara ya bidhaa duniani ilipata mwelekeo wa kupanda zaidi katika nusu ya kwanza ya Mwaka 2024, ikionyesha ongezeko la mwaka hadi mwaka la asilimia 2.3. Ripoti hiyo inasema, ukuaji huo unatarajiwa kufuatiwa na upanuzi zaidi wa wastani katika kipindi kilichobaki cha mwaka huu na hadi ifikapo Mwaka 2025.
Ukuaji wa jumla wa bidhaa za ndani duniani kwa kiwango cha mabadilishano ya fedha cha soko unatarajiwa kubaki tulivu kwenye asilimia 2.7 katika Mwaka 2024 na 2025, imesema ripoti hiyo.
WTO imesema kuwa kufikia katikati ya Mwaka 2024, mfumuko wa bei ulikuwa umepungua vya kutosha kuwezesha benki kuu kupunguza viwango vya riba ambapo kushuka huko kwa mfumuko wa bei kunatarajiwa kuongeza mapato halisi ya kaya na kuchochea matumizi ya watumiaji, wakati viwango vya chini vya riba vinapaswa kuhamasisha kampuni kuongeza matumizi yao ya uwekezaji.
Ripoti hiyo pia imetahadharisha kuwa sera zinazotofautiana za kifedha kati ya nchi zenye uchumi mkubwa zinaweza kusababisha kuyumba kwa mambo ya fedha na kuhama kwa mtiririko wa mtaji wakati benki kuu za nchi mbalimbali zikipunguza viwango vya riba. Imesema, hali hiyo inaweza kufanya ulipaji wa madeni kuwa mgumu zaidi, haswa kwa nchi duni kiuchumi.
"Tunatarajia kuimarika taratibu kwa biashara ya kimataifa katika Mwaka 2024, lakini tunaendelea kuwa macho kwa uwezekano wa kukatisha tamaa, hasa uwezekano wa kuongezeka kwa migogoro ya kikanda kama ile ya Mashariki ya Kati," Mkurugenzi Mkuu wa WTO Ngozi Okonjo-Iweala amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma