Lugha Nyingine
Meli ya kwanza kutoka Bandari ya Chancay ya Peru yafika Shanghai,?China (3)
SHANGHAI - Meli ya "Xin Shanghai," inayoendeshwa na Kampuni ya Usafiri wa Majini ya COSCO ya China, imewasili katika Bandari ya Yangshan mjini Shanghai, Mashariki mwa China majira ya 9:30 alasiri jana Jumatano baada ya safari ya siku 23 kutoka Bandari ya Chancay ya Peru, ikiwa ni meli ya kwanza kuwasili Shanghai kutoka Chancay baada ya bandari hiyo ya Peru kufunguliwa rasmi mwezi Novemba.
Safari hiyo pia inaonyesha kuanzishwa kwa uendeshaji wa safari za baharini kati ya Shanghai na Bandari hiyo ya Chancay, mradi uliozinduliwa hivi karibuni wa ushirikiano wa Ukanda Mmoja, Njia Moja kati ya China na Peru.
Mizigo iliyo ndani ya meli hiyo ni pamoja na bidhaa mbalimbali za Peru, kama vile bluberi, parachichi na bidhaa za madini.
Kwa mujibu wa Wu Jianzhong, meneja wa kikanda wa Kampuni ya Joy Wing Mau Fruit Technologies (JWM), mmiliki wa bluberi hizo za Peru zilizoko kwenye meli hiyo, nusu ya bluberi hizo zitasambazwa mjini Shanghai, zikilenga masoko ya jumla na supamaketi mashariki mwa China, wakati zilizobaki zitasafirishwa hadi kaskazini mwa China.
Kabla ya kufunguliwa kwa bandari hiyo ya Chancay, biashara kati ya Peru na China ilipitia Bandari ya Callao ya Peru. Baada ya Bandari ya Chancay kufanya kazi, huduma zaidi za usafirishaji wa makontena zimeanzishwa katika pwani ya magharibi ya Amerika Kusini, ikipunguza muda wa usafirishaji kati ya Peru na China hadi siku karibu 23 – ikiwa ni haraka zaidi kuliko wastani wa soko wa sasa.
Kuanzishwa kwa njia hiyo mpya kunasaidia matunda freshi ya Peru na bidhaa nyinginezo kuingia katika masoko ya China na Asia-Pasifiki.
Njia hiyo mpya ya moja kwa moja kati ya Bandari za Chancay na Shanghai itasaidia kujenga mtandao wa biashara wenye ufanisi na unganishi zaidi, ukiunganisha mikoa ya pwani na maeneo ya barani ya Peru, pamoja na nchi nyingine za Latini Amerika, amesema Chen Xiaochen, meneja wa biashara wa kampuni hiyo ya usafirishaji ya COSCO tawi la Latini Amerika.
Njia hiyo ni alama muhimu katika mkakati mpana wa China wa kuimarisha muunganisho wa mawasiliano ya bahari duniani, ikionyesha kuongezeka kwa mchango wa nchi hiyo katika kujenga mtandao wa biashara wa kimataifa ulio jumuishi na wenye ufanisi zaidi, Chen ameongeza.
Ikiwa ni bandari ya kwanza ya kisasa na ya kijani katika Amerika Kusini, Bandari hiyo ya Chancay, iliyozinduliwa mwezi Novemba, iko umbali wa kilomita karibu 78 kaskazini mwa Lima, mji mkuu wa Peru.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma