Lugha Nyingine
Simulizi ya Picha: Mwanafunzi wa Rwanda Ajikita Kwenye Utafiti wa Mahindi Nchini China (4)
Gatera, Mnyarwanda mwenye umri wa miaka 31, ni mwanafunzi wa PhD katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Anhui, na kozi yake ni kuotesha mbegu za mahindi. Mwaka 2019, Gatera alikuja Hefei, Mkoa wa Anhui kusoma shahada ya uzamili kwa ufadhili wa serikali ya China na kuendelea masomo yake ya shahada ya uzamivu katika chuo kikuu hicho.
Wakati wa likizo ya majira ya joto, Gatera na wanafunzi wenzake walifanya majaribio katika maabara, wakifuatilia sampuli za chavua na kukusanya data za majaribio. Kwa kupitia utafiti kuhusu athari za joto na ukame kwa chavua ya mahindi, Gatera alijikita katika kuendeleza aina mpya ya mahindi yenye uvumilivu kwa ukame na joto. Anaamini kwamba utafiti huu una umuhimu mkubwa katika muktadha wa kuongezeka kwa hali ya hewa ya joto duniani.
"Katika maskani yangu Rwanda, mahindi ni mojawapo kati ya mazao makuu, lakini teknolojia ya kilimo iko nyuma kidogo. China ina teknolojia ya hali ya juu na kupenda kunufaika pamoja na nchi nyingine. Nataka kurudi maskani yangu pamoja na uzoefu niliopata hapa China na kuchangia maendeleo ya kilimo huko," Gatera alisema.
Gatera anamchukulia mwanasayansi mashuhuri wa China Yuan Longping kuwa mfano wake wa kuigwa, akiamini kwamba kazi ya Yuan Longping na mpunga chotara imetatua matatizo ya usalama wa chakula katika sehemu nyingi duniani, na amewatia moyo watafiti vijana wengi kama yeye. "Natumai kwamba kupitia utafiti wangu, Afrika inaweza kuzalisha nafaka nyingi zaidi na kuboresha maisha ya watu," Gatera alisema.?
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma